2 Corinthians 5

Makao Yetu Ya Mbinguni

1 aKwa maana twajua kama hema yetu ya dunia tunayoishi ikiharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba iliyo ya milele kule mbinguni, isiyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 2Katika hema hii twalia kwa uchungu, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni, 3kwa kuwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tena kuwa uchi. 4 bKwa kuwa tukiwa bado katika hema hii twalia kwa uchungu na kulemewa, kwa sababu hatutaki kuvuliwa bali kuvikwa makao yetu ya mbinguni ili kwamba kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima. 5 cBasi Mungu ndiye alitufanya kwa ajili ya jambo lilo hilo naye ametupa Roho Mtakatifu kuwa amana, akituhakikishia ahadi ya kile kijacho.

6 dKwa hiyo siku zote tunalo tumaini, hata ingawa tunajua kwamba wakati tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na Bwana, 7 ekwa maana twaenenda kwa imani wala si kwa kuona. 8 fNaam, tunalo tumaini na ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana. 9 gKwa hiyo, kama tuko katika mwili huu au tuko mbali nao, lengo letu ni kumpendeza Bwana. 10 hKwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Al-Masihi, ili kila mmoja apate kulipwa kwa ajili ya yale ambayo yametendwa katika mwili wake, yakiwa mema au mabaya.

Huduma Ya Upatanisho

11 iBasi, kwa kuwa tunajua kumcha Bwana, tunajitahidi kuwavuta wengine. Lakini Mungu anatufahamu dhahiri, nami natumaini kwamba tu dhahiri katika dhamiri zenu pia. 12 jSio kwamba tunajaribu kujistahilisha kwenu tena, lakini tunataka kuwapa nafasi ili mwone fahari juu yetu mweze kuwajibu hao wanaoona fahari juu ya mambo yanayoonekana badala ya mambo yaliyo moyoni. 13 kKama tumerukwa na akili, ni kwa ajili ya Mungu; kama tuna akili timamu, ni kwa ajili yenu. 14 lKwa kuwa upendo wa Al-Masihi unatutia nguvu, kwa sababu tunasadiki kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote, kwa hiyo wote walikufa. 15 mNaye alikufa kwa ajili ya watu wote, ili kwamba wote wanaoishi wasiishi tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuliwa tena kwa ajili yao.

16 nHivyo tangu sasa hatumwangalii mtu yeyote kwa mtazamo wa kibinadamu. Ingawa wakati fulani tulimwangalia Al-Masihi kwa namna ya kibinadamu, hatumwangalii tena hivyo. 17 oKwa hiyo kama mtu akiwa ndani ya Al-Masihi, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya. 18 pHaya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kwa njia ya Isa Al-Masihi na kutupata sisi huduma ya upatanisho: 19Kwamba Mungu alikuwa ndani ya Al-Masihi akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, akiwa hawahesabii watu dhambi zao. Naye ametukabidhi sisi ujumbe huu wa upatanisho. 20 qKwa hiyo sisi ni mabalozi wa Al-Masihi, kana kwamba Mungu anawasihi kupitia kwa vinywa vyetu. Nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Al-Masihi, mpatanishwe na Mungu. 21 rKwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kwake yeye.
Copyright information for SwhKC